Mwanasiasa wa upinzani nchini Afrika Kusini, Julius Malema, amehukumiwa kifungo cha miaka mitano jela baada ya kupatikana na hatia ya kufyatua risasi hewani wakati wa mkutano wa hadhara, mahakama hiyo imetoa uamuzi huo leo Alhamisi April 16,2026.
Malema (45), ambaye ni miongoni mwa wanasiasa maarufu zaidi nchini humo, alipatikana na hatia mwaka jana kwa makosa matano, ikiwemo kumiliki silaha kinyume cha sheria na kufyatua risasi katika eneo la umma. Tukio hilo lilitokea mwaka 2018 katika uwanja wa michezo ulioko jimbo la Eastern Cape.
Mara tu baada ya hukumu hiyo kusomwa katika mahakama ya KuGompo City (zamani East London), mawakili wa Malema waliwasilisha ombi la kukata rufaa kupinga uamuzi huo.
Iwapo hukumu hiyo itathibitishwa baada ya rufaa zote kukamilika, Malema hataruhusiwa kuendelea kuwa mbunge. Hali hiyo itakuwa pigo kubwa kwa chama chake cha siasa za mrengo wa kushoto, Economic Freedom Fighters (EFF), ambacho kinaungwa mkono kwa kiasi kikubwa na vijana wa Afrika Kusini wanaokasirishwa na pengo la kiuchumi na kijamii lililoendelea kuwepo tangu kumalizika kwa utawala wa ubaguzi wa rangi mwaka 1994.
