
Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha linawashikilia watu sita kwa tuhuma za kuhusika katika mauaji ya Askari Polisi Roland Mollel, yaliyotokea usiku wa Aprili 15, 2026, katika mtaa wa Mlimani, kata ya Muriet, Jijini Arusha.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Justine Masejo, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo la kusikitisha, akisema kuwa Askari Mollel alikuwa akitekeleza shughuli zake binafsi baada ya kumaliza kazi, ambapo alishambuliwa na kundi la watu waliokuwa wakidai kuwapo kwa wezi katika eneo lao.
Kwa mujibu wa Kamanda Masejo, wakati Askari Mollel akiwa anapita kwa pikipiki na dereva bodaboda, kundi hilo lilianza kuwashambulia kwa kumpiga na kumkimbiza, hali iliyosababisha kifo cha askari huyo.
Polisi mkoani Arusha wamesema wanaendelea na msako mkali wa kuwatafuta watuhumiwa wengine wanaohusishwa na tukio hilo, huku uchunguzi ukiendelea. Kamanda Masejo pia ametoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kuchukua sheria mikononi kwa kuongozwa na mihemko, kwani hiyo ni kinyume cha sheria na inaweza kusababisha madhara kwa watu wasiokuwa na hatia.
Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi wa Arusha kuendelea kutoa ushirikiano katika suala hili na kuwa makini na tabia za kutaka kujichukulia sheria mikononi. “Tutahakikisha sheria inachukuliwa kwa umakini, na tutahakikisha wahusika wanawajibika kwa vitendo vyao,” alisema Kamanda Masejo.
Tukio hili limeibua maswali kuhusu usalama katika maeneo ya miji na umhimu wa ushirikiano kati ya wananchi na vyombo vya ulinzi katika kukabiliana na uhalifu. Polisi wamesisitiza kuwa, wakati wa kutatua changamoto za kijamii, ni muhimu kuwa na uelewa na ushirikiano kwa jamii nzima.

SHARE THIS:
