
Familia ya Ashly Robinson, anayejulikana pia kama Ashlee Jenae, inaendelea kukabiliana na mshtuko mkubwa kufuatia kifo chake cha ghafla huku pia ikikabiliwa na changamoto za kifedha za kuurejesha mwili wake nchini Marekani.
Baba yake, Harry Robinson, ameanzisha kampeni ya GoFundMe yenye lengo la kukusanya dola 50,000, akieleza kuwa fedha hizo zitatumika kugharamia safari, maandalizi ya mazishi na gharama nyingine zinazoongezeka wakati familia ikiendelea kushirikiana na uchunguzi unaoendelea nje ya nchi.

Mpa ka leo Famili hiyo imefanikiwa kupata kiasi cha $39,976 sawa na Milioni 101 kwa pesa za Kitanzania bado wanaendelea kupokea michango kufikia lengo lao.
Ashly Robinson alikutwa akiwa hana fahamu katika villa ya ZURI iliyopo Nungwi, Wilaya ya Kaskazini ‘A’, Unguja, Zanzibar na baadaye alikimbizwa hospitalini ambako alitangazwa kufariki dunia Ijumaa, Aprili 10.
Tukio hilo limeiacha familia ikiwa katika majonzi makubwa na pia limefungua uchunguzi rasmi wa mamlaka za eneo husika.
Ripoti za awali zinaeleza kuwa polisi wanachunguza uwezekano mbalimbali, ikiwemo kujidhuru (suicide), ingawa hakuna hitimisho rasmi lililotolewa hadi sasa. Aidha, mamlaka zinasema marehemu alihusishwa na mgogoro na mchumba wake, Joe McCann, kabla ya kifo chake. Inaripotiwa kuwa wahudumu wa hoteli waliingilia kati na kuwatenganisha wawili hao na kuwapeleka vyumba tofauti, tukio ambalo sasa ni sehemu ya uchunguzi unaoendelea.
Wakati uchunguzi ukiendelea, familia inaendelea kusubiri majibu ya kina kuhusu kilichotokea huku ikiomba msaada wa umma kukamilisha gharama za kurejesha mwili wake nyumbani.
