Serikali imepokea rasmi hoja iliyowasilishwa na Mbunge wa Jimbo la Kisarawe, Dkt. Selemani Jafo, kuhusu kuanzishwa kwa mfumo wa ajira za muda (part-time) kwa vijana wasomi ambao bado hawajapata ajira rasmi nchini.
Akiwasilisha hoja hiyo bungeni, Dkt. Jafo alipendekeza kuwa Serikali iweke utaratibu maalum wa kuwaajiri vijana hao kwa mikataba ya muda, huku wakilipwa kati ya shilingi laki tano (500,000) hadi laki saba (700,000) kwa mwezi. Alisisitiza kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza tatizo la ajira, kuwajengea uzoefu wa kazi, na kuwawezesha vijana kujitegemea kiuchumi.
Hoja hiyo imepokelewa leo bungeni wakati wa kuhitimisha mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, ambapo Serikali imeonesha utayari wa kuichakata kwa kina kabla ya kufikia maamuzi ya utekelezaji.
Wachambuzi wa masuala ya uchumi wanaona pendekezo hilo linaweza kuwa suluhisho la muda mfupi lenye tija kwa vijana wengi, hasa katika kipindi hiki ambapo changamoto ya ajira imeendelea kuwa kubwa nchini.
Lengo kuu la hoja hiyo ni kuimarisha ushiriki wa vijana katika shughuli za uzalishaji, kuongeza ujuzi wa vitendo, pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia nguvu kazi ya wasomi.
