Mgombea ubunge jimbo la Kigoma mjini kupitia ACT Wazalendo @actwazalendo_official Zitto Kabwe ameahidi kuwa chama chake kitakaposhinda nafasi ya ubunge na pamoja na kuwa na madiwani wengi kisha kuongoza Halmashauri ya Kigoma Ujiji kitaondoa michango yote mashuleni katika manispaa hiyo ambayo siyo rasmi.
Zitto ametoa kauli hiyo jana, Oktoba 26, 2025 akiwa katika kata ya Mwanga kusini, alipohitimisha kampeni zake za kata kwa kata, ambapo amefanikiwa kuzifikia kata zote 19 za jimbo hilo.
Akiwa katika kata hiyo, Zitto amesema manispaa hiyo ikiwa chini ya chama chake itapitia michango yote iliyopo mashuleni na kuiondoa ili kupunguza mzigo kwa wazazi wanaosomesha watoto wao katika manispaa hiyo.
“Haiwezekani wewe mzazi umlipe mlizi anayelinda shule, ulipie umeme wa shule, kazi ya serikali ni nini? tutakomesha haya mambo, tutaondoa michango yote ambayo ni kero”, alisema Zitto
Aidha katika kuboresha sekta ya elimu katika
manispaa hiyo, Zitto ameahidi kuanzisha shule mpya za sekondari na kupandisha hadhi shule nne kuwa na kidato cha tano na cha sita katika manispaa hiyo.
“Tunataka tuwe na shule za ‘high school’ nne ndani ya mji wetu mbili za sayansi na nyingine za sanaa na tuongeze idadi ya shule za sekondari ili watoto wetu wapate elimu wanayostahiki”, aliongeza Zitto
Zitto amewataka wananchi wa manispaa hiyo kutodanganyika na kauli zinazotweza elimu, kwa kuwa elimu ndio silaha ya kuondokana na umaskini kama ilivyoandikwa kwenye vitabu vya dini.
