JESHI la Marekani limefanya mashambulizi kadhaa ya kile lilichokiita mashambulizi ya “kujilinda” dhidi ya malengo ya kijeshi ya Iran mwishoni mwa wiki, baada ya ndege yake isiyo na rubani kudunguliwa juu ya maji ya kimataifa, katika tukio jipya linaloongeza mvutano wa kijeshi kati ya Washington na Tehran na kuzua hofu ya kuongezeka kwa mapigano katika ukanda wa Mashariki ya Kati.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na United States Central Command (CENTCOM), mashambulizi hayo yalifanyika siku za Jumamosi na Jumapili na yalilenga maeneo ya kijeshi ndani ya Iran yanayohusishwa na mifumo ya rada, udhibiti wa drones pamoja na miundombinu ya ulinzi wa anga ambayo Marekani inadai ilitumika katika shughuli za kijeshi zilizokuwa zikitishia usalama wa vikosi vyake na usafiri wa majini wa kimataifa.
CENTCOM ilisema mashambulizi hayo yalielekezwa katika maeneo ya Goruk, Iran pamoja na Kisiwa cha Qeshm, eneo la kimkakati lililopo karibu na Mlango wa Hormuz, njia muhimu sana ya usafirishaji wa mafuta duniani. Kisiwa hicho kimekuwa kikitajwa mara kwa mara katika mivutano ya kijeshi kwa sababu ya nafasi yake muhimu katika shughuli za kijeshi na biashara ya baharini katika Ghuba ya Uajemi.
Katika taarifa yake, jeshi la Marekani lilisema hatua hiyo ilifuatia kudunguliwa kwa ndege yake aina ya MQ-1 drone, ambayo ilidai ilikuwa ikiendesha operesheni juu ya maji ya kimataifa wakati iliposhambuliwa. Marekani imeishutumu Iran kwa kile ilichokiita “uchokozi wa moja kwa moja,” ikisema ndege hiyo haikuwa imeingia katika anga ya Iran na ilikuwa ikifanya kazi kwa mujibu wa sheria za kimataifa.
