Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Agape, Dkt. Vernon Fernandes, ametoa wito kwa Watanzania wote kuendelea kudumisha amani na kulinda rasilimali zilizopatikana chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, akisema kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi kinapaswa kuwa cha tafakari na siyo vurugu.
Akizungumza Jumatatu, Oktoba 27, 2025, katika Kongamano la Amani la Kitaifa kuelekea Uchaguzi Mkuu lililofanyika katika Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam, Dkt. Fernandes amesema taifa limepiga hatua kubwa za maendeleo katika kipindi cha miaka minne na nusu ya uongozi wa Rais Samia, hivyo ni wajibu wa kila Mtanzania kulinda rasilimali na amani iliyopo.
Amesisitiza kuwa mafanikio hayo hayawezi kudumu endapo wananchi hawatakuwa tayari kuyatetea kwa amani na uadilifu, hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi.
Mchungaji Fernandes ameonya dhidi ya watu wanaotabiri vurugu au machafuko wakati wa uchaguzi, akisema taasisi za usalama zipo kuhakikisha utulivu unadumu nchini.
“Unajua kuna watu wanaweza kusema kuwa kutakuwa na fujo, lakini nashukuru kwamba polisi wako pale — kazi ya polisi ni kuhakikisha kwamba kunakuwepo kwa amani,” amesema.
Kongamano hilo lililobeba kaulimbiu “Kupiga Kura ni Haki Yetu, Kulinda Amani ni Wajibu Wetu”, limehudhuriwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, ambaye amemwakilisha Mgeni Rasmi, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango.
