Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Dkt. Abubakar Bin Zubeir Ally amewataka Watanzania kuipa kipaumbele amani ya taifa, akisisitiza kuwa mifano ya mataifa jirani yanayokabiliwa na migogoro inapaswa kuwa somo la kutosha kwa kila mmoja kutambua thamani ya utulivu wa nchi.
Akizungumza leo Jumatatu, Oktoba 27, 2025, katika Kongamano la Amani la Kitaifa kuelekea Uchaguzi Mkuu, lililofanyika jijini Dar es Salaam chini ya kaulimbiu “Kupiga Kura ni Haki Yetu, Kulinda Amani ni Wajibu Wetu,” Mufti Abubakar amesema uharibifu wa nchi haupaswi kukumbatiwa kwa kisingizio chochote.
“Tuweke suala la amani mbele katika nchi yetu. Kwa mifano iliyokuwa wazi wala haina haja ya kuelezwa mtu kwa undani. Ukigeuza uso kulia au kushoto, ukatazama nchi za karibu au kupitia vyombo vya habari utaona kwamba jambo baya halifai kukubaliwa na kukumbatiwa katika nchi. Masilahi ya watu ndio yenye kutangulizwa, uharibifu wa nchi hautakiwi, tutangulize amani,” amesema Mufti Abubakar.
Kongamano hilo limefanyika katika Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), na mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango, aliyewakilishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo.
