Rais wa Cameroon, Paul Biya, amechaguliwa tena kuongoza taifa hilo kwa muhula wa 8 baada ya kupata asilimia 53.66 ya kura zilizopigwa. Kutangazwa kwake kumeibua hali ya taharuki na kusababisha uwezekano wa makabiliano na wafuasi wa mgombea mkuu wa upinzani, Issa Tchiroma Bakary, ambaye amedai kuwa ndiye mshindi halali wa uchaguzi huo.
Matokeo ya uchaguzi wa Cameroon yametolewa leo Oktoba 27, 2025 chini ya Tume ya uchaguzi nchini humo, iliyoyatangaza ikiwa ni saa kadhaa baada ya watu wanne kuripotiwa kupoteza maisha kutokana na maandamano ya wananchi, yaliyoitishwa na kiongozi wa upinzani, Issa Tchiroma Bakary.
Baada ya kutangazwa kwa matokeo, kiongozi huyo wa upinzani ambaye awali alidai kuwa ameshinda uchaguzi huo, ameandika kwenye ukurasa wake wa Facebook kwamba silaha zimeelekezwa kwa raia waliokusanyika nje ya nyumba yake katika mji wa Garoua, kaskazini mwa nchi hiyo, ili kuzuia mkusanyiko.
Wiki moja kabla ya kutangazwa kwa matokeo rasmi, waandamanaji wa upinzani walikabiliana na vikosi vya usalama kufuatia ripoti za vyombo vya habari vya ndani zilizoashiria kuwa Biya alikuwa akielekea kushinda uchaguzi wa Oktoba 12, ingawa kwa wakati huo Serikali ilikanusha vikali tuhuma za upinzani kuhusu udanganyifu wa kura.
Paul Biya, mwenye umri wa miaka 92, amekuwa madarakani tangu mwaka 1982. Mwaka 2008, aliondoa kikomo cha muhula wa urais, hatua iliyomruhusu kuendelea kugombea.
Kwa sasa, Biya ndiye kiongozi aliyekaa madarakani kwa muda mrefu zaidi.
