
Waziri mkuu wa Sudan Abdallah Hamdok ametangaza kujiuzulu wadhifa huo.
Hatua hiyo ya Hamdok ameitangaza jana Jumapili ikiwa ni wiki sita tangu aliporejeshwa madarakani baada ya mapinduzi ya kijeshi ya mwezi Oktoba mwaka jana yaliyoiondosha serikali ya kiraia.
Akitangaza hatua hiyo kupitia televisheni, Hamdok amesema anaachia wadhifa huo ili kuruhusu mtu mwingine kusaidia taifa hilo kuvuka kipindi cha mpito cha mabadilishano ya kidemokrasia ya madaraka.
Aidha, ametoa mwito wa kufanyika kwa majadiliano ili kufikiwa kwa makubaliano mapya kuhusiana na namna serikali hiyo mpya itakavyofikiwa.
Kuondoka kwa Hamdok kunatafsiriwa kuwa pigo kubwa na huenda taifa hilo likaingia kwenye mzozo mkubwa zaidi, ikiwa ni miaka mitatu baada ya vuguvugu lilimuondoa madarakani aliyekuwa kiongozi wa taifa hilo Omar al-Bashir.
