Smart glasses (miwani janja) zinazoweza kurekodi video, kupiga picha na kunasa sauti bila mtumiaji kushika simu zimeanza kuzua mjadala kuhusu faragha, huku baadhi ya baa, migahawa na kumbi za sinema na maonyesho nchini Uingereza zikianza kuzuia matumizi yake.
Kampuni ya EssilorLuxottica, mshirika wa Meta katika utengenezaji wa miwani hiyo, imesema jozi milioni saba ziliuzwa duniani mwaka 2025.
Takwimu za kampuni ya utafiti wa soko Counterpoint Research zinaonyesha usafirishaji wa miwani mahiri uliongezeka kwa asilimia 212 katika nusu ya kwanza ya mwaka 2026, huku Meta ikiongoza soko kwa takribani asilimia 84.
Wasiwasi umeongezeka baada ya kusambaa kwa video zinazoonyesha watu wakirekodi wengine bila ridhaa yao, hasa wanawake.
Baadhi ya wakazi wa London wanasema wanahisi kutokuwa salama katika maeneo ya kijamii ambako wanatarajia faragha.
Mlolongo wa baa za Wetherspoons umepiga marufuku wateja kurekodi video kwa kutumia miwani hiyo.
Uongozi wake umesema msimamo wao ni kuhakikisha kamera zinazimwa.
Kampuni ya Meta imesema miwani yake ina taa inayoashiria kurekodi, na imechukua hatua kuzuia watumiaji kuifunika taa hiyo wakati wa kurekodi.
Katika kumbi za maonyesho, kampuni ya ATG Entertainment imesema watazamaji watakaobainika kutumia miwani hiyo wataombwa kuivua na kufuta video walizorekodi.
Chama cha Sinema nchini Uingereza pia kimesema baadhi ya kumbi zimepiga marufuku matumizi yake kutokana na hofu ya kurekodi na kusambaza filamu kinyume cha sheria.
Wataalamu wa haki za binadamu na faragha wanaonya kuwa teknolojia hiyo inafanya iwe vigumu kutambua mtu anayerekodi, huku sheria zilizopo zikikabiliwa na changamoto ya kwenda sambamba na maendeleo ya teknolojia.
Hata hivyo, mashirika yanayotetea watu wenye ulemavu wa kuona yanaonya dhidi ya marufuku ya jumla, yakisema miwani hiyo inaweza kuwasaidia kusoma alama za barabarani, menyu za migahawani na kutambua mazingira yanayowazunguka.
Mjadala huo unaendelea wakati kampuni za teknolojia zikiwekeza zaidi katika miwani mahiri, zikilenga kuifanya kuwa kifaa muhimu cha mawasiliano na matumizi ya akili mnemba (AI).
