
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amesema mradi wa ujenzi wa bandari ya uvuvi utakaoanza hivi karibuni wilayani Kilwa, mkoani Lindi, utachochea ukuaji wa uchumi wa bluu na kupelekea kuongezeka kwa pato la taifa.
Ndaki ameyasema hayo wakati wa hafla fupi ya utiaji saini nyaraka za makubaliano ya ujenzi wa bandari hiyo baina ya Serikali na Kampuni ya ujenzi ya China Habour Engineering Company (CHEC) iliyofanyika jijini Dodoma, jana Juni 7, 2022.
Amesema anamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kujenga bandari hiyo kwa fedha za ndani huku akiongeza kuwa kukamilika kwake kutakuwa na faida nyingi za kiuchumi kwa wavuvi, wananchi na taifa kwa ujumla.
“Namshukuru Rais Samia kwa kukubali kufanya jambo hili ambalo lilikuwa ndoto sasa kuwa kweli, amekubali kutoa sh. za Kitanzania bilioni 266.79 kwa ajili ya ujenzi wa bandari hii pamoja na miundombinu mingine ikiwamo soko la kisasa la samaki,” amesema.
Ameongeza kuwa bandari hiyo ikikamilika itakuwa na uwezo wa kuhifadhi tani 60,000 kwa mwaka za mazao ya uvuvi kutoka ukanda wa bahari ya Hindi huku akisisitiza kuwa bandari hiyo itakuwa kubwa kuliko zote zilizopo Pwani ya Afrika Mashariki.
Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Dk. Christine Ishengoma, ameihimiza Wizara hiyo kuhakikisha inamsimamia vema mkandarasi aliyekabidhiwa kujenga bandari hiyo huku akiongeza kuwa wao kama kamati watakuwa wanafuatilia kwa karibu kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati ili Watanzania waone matunda ya fedha zao.
