*Msaada wa chakula ukikosekana mamia wanaweza kufa kwa njaa

Umoja wa Mataifa (UN), umesema Somalia inaelekea kwenye baa la njaa huku nchi hiyo ikikabiliwa na ukame mbaya zaidi kuwahi kutokea katika takriban miongo minne.
Kwa sasa, karibu nusu ya watu wanakabiliwa na uhaba wa chakula.
Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu nchini humo, Adam Abdelmoula, amesema jumuiya ya kimataifa lazima ichukue hatua sasa au watu zaidi watakufa.
Amesema nchi iko kwenye ukingo wa njaa mbaya ambayo inaweza kuchukua mamia ya maelfu ya maisha.
Misimu minne ya mvua mfululizo imeshindwa na Umoja wa Mataifa unakadiria ukame mkali uliofuata umeathiri watu milioni saba na wengine zaidi ya 800,000 kuyahama makazi yao.
Wakati huo huo, bei ya vyakula inapanda kwa kiasi kwa sababu ya vita nchini Ukraine – na usaidizi wa kibinadamu haupatikani kwa wengi kwa sababu ya ukosefu wa usalama na migogoro.
Mifugo milioni tatu, ambayo ni chanzo kikuu cha maisha, imekufa kutokana na ukame. Abdelmoula amesema mwitikio kutoka jumuia ya kimataifa kufikia sasa haujatosha.
Mwaka 2011, ukame mkali ulisababisha njaa iliyoua watu robo milioni.
