
Rais wa Angola Joao Lourenco anatarajiwa kusalia madarakani, baada ya chama chake kuongoza katika uchaguzi uliokuwa na ushindani mkali katika historia ya demokrasia ya nchi hiyo, wakati karibu kura zote zikiwa zimehesabiwa.
Matokeo yaliyotangazwa na tume ya taifa ya uchaguzi yameonesha chama tawala cha the People’s Movement for the Liberation of Angola (MPLA), kinaongoza kwa asilimia 51.7 ya kura huku asilimia 97 ya kura zikiwa zimekwisha hesabiwa.
Kura hizo ni ndogo sana ikilinganishwa na ushindi wake wa awali wa asilimia 61 ya kura zote.
Chama kikuu cha upinzani, the National Union for the Total Independence of Angola (UNITA) kinachoongozwa na Adalberto Costa Junior, kilipata asilimia 44.05, ikiwa ongezeko kubwa kutoka asilimia 26.67 kilizopata katika uchaguzi wa 2017.
Ofisa mwandamizi wa chama cha UNITA ameuambia mkutano wa waandishi wa habari kwamba matokeo rasmi hayalingani na hesabu zao.
“Tunatumai kunaweza kuwa na busara, hatuhamasishi uasi, mchakato haujamalizika, lazima tuwe watulivu,” amesema Anastacio Ruben Sicato.
