Jumuiya ya Kimataifa imetoa mwito wa kuzingatia utulivu baada ya mapigano kuanza tena Kaskazini mwa Ethiopia kati ya vikosi vya serikali na waasi wa Tigray.
Mapigano hayo yameuvunja mpango uliokuwapo wa kuweka chini silaha na kutilia kiwingu matumaini ya kupatikana Amani.
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani Antony Blinken amesema makubaliano ya kusitisha vita yaliyofikiwa na pande zinazopigana mwezi Machi yalikuwa yamepunguza machafuko na kuokoa maisha.
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell amezihimiza pande zote kujiondoa katika hali hiyo inayoweza kuzusha vita kamili.
Mabalozi wa Uingereza, Uturuki, Umoja wa Afrika, na jumuia ya kibiashara ya Afrika Mashariki ya IGAD wametoa miito sawa na hiyo ya kuzitaka pande zote kujizuia na kufanya mazungumzo ya amani.
