
Sehemu ya vijana waliohudhuria Mdahalo huo ulioandaliwa na shirika la AMDT kuhusu upatikanaji mitaji na kukuza shughuli za kilimo biashara kwa vijana.
Serikali imesema imeendelea kufanya jitihada za kuweka mazingira wezeshi kwa vijana kuweza kujikwamua kiuchumi kwa kutoa mikopo kwa kijana mmoja mmoja na si kwa makundi kama ilivyokuwa awali.
Naibu Waziri- Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi ametoa kauli hiyo jana Septemba 15, 2022, wakati akifungua rasmi Mdahalo wa Vijana Kuhusu Upatikanaji wa Mitaji na Kukuza Shughuli za Kilimo Biashara kwa Vijana.
Amefafanua kuwa muongozo mpya uliotolewa umerahisisha sifa za kukopa kwa vijana kulingana na mahitaji yao.
Naibu Waziri Katambi ameendelea kubainisha kuwa yapo maboresho ya mifumo katika kila sekta zinazoshughulikia masuala ya vijana ambayo itasaidia kuleta mazingira wezeshi kujikwamua kiuchumi na kuweza kujiajiri.
Ameongeza kuwa Serikali imeendelea kushirikiana na Sekta Binafsi katika kutoa mafunzo kwa vijana ili kuweza kutatua changamoto za kiuchumi.
Aidha amesisitiza kuwa mafunzo hayo yanasaidia kuongeza maarifa, ujuzi na mipango thabiti kwa vijana kuweza kutambua vipaji vyao.
“Tunafurahi kwamba leo katika mdahalo huu uliotolewa na shirika AMDT (AGRICATURAL MARKERT DEVELOPMENT TRUST), umetupa fursa nyingine ya kusikiliza changamoto, vipaumbele, uzoefu na matarajio kutoka kwa vijana wote wa kike na kiume.wanaofanya shughuli zao za kiuchumi katika sekta ya kilimo.
Amesisitiza kuwa vijana waliopata mafunzo hayo waendelee kushirikiana na wengine ili kubadili mitazamo na kushirikiana na Serikali kukabiliana na changamoto zinazowakabili.
