
Serikali imesema haina mpango wa kubadili utaratibu uliowekwa kwa askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), wa kukaa miaka sita bila kuoa ama kuolewa mara baada ya kujiunga na jeshi hilo.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa (JKT), Dk. Stergomena Tax ameliambi Bunge kuwa kwa sasa utaratibu huo utabakia kama ulivyo kutokana na misingi iliyowekwa kwa ajili ya kuwaandaa askari hao kulinda nchi.
Dk. Stergomena amesema askari wapya wanaojiunga na Jeshi wanahesabiwa kama wapiganaji ambao wanapaswa kupewa ujuzi zaidi na kutumika kwenye vita hivyo miaka sita iliyowekwa ya kutokuoa ama kuolewa na inatoa nafasi kwa askari hao kutumika katika shughuli za medani.
Waziri huyo alikuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Bunda, Boniface Getere aliyehoji iwapo kuna uwezekano kwa serikali kupunguza kutoka miaka sita iliyopo sasa kwa askari wapya wa Jeshi hilo kuoa ama kuolewa na kuwa mwaka mmoja ama miaka miwili.
