
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (kulia), akizungumza na Makamu Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Monique Nsanzabaganwa katika ofisi za Wizara hiyo jijini Da es Salaam juzi Septemba 14, 2022.
Makamu Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Monique Nsanzabaganwa, ameipongeza Tanzania kwa kuwa miongoni mwa wadau muhimu katika Umoja huo.
Monique ametoa pongezi hizo alipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula pembezoni mwa Mkutano wa Wanawake na Vijana katika Biashara kwenye Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA), uliofanyika Septemba 12 hadi 14, 2022 jijini Dar es Salaam.
Akifafanua shughuli za utekelezaji zinazofanywa na Kamisheni ya Umoja wa Afrika kwa kushirikiana na Nchi Wanachama, Monique alisema Tanzania licha ya nafasi yake ya kuunga mkono uanzishwaji wa umoja huo pia imekuwa ikikamilisha michango yake ya uanachama kwa wakati.
“Ukamilishaji wa michango kwa wakati kutoka kwa Nchi wanachama unawezesha uendeshaji wa shughuli za Sekretarieti kutekelezeka kwa tija na kusaidia kupatikana kwa maslahi ya watumishi,” alisema.
Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata amemuhakikishia kuwa Tanzania itaendelea kuheshimu makubaliano yaliyokubaliwa katika Umoja wa Afrika sanjari na kuhakikisha inanufaika na fursa mbalimbali kama ajira na biashara zinazopatikana.
Pia ameshukuru kwa jitihada zinazofanywa na Umoja wa Afrika kupitia Mkataba wa AfCFTA kwa kumtambua Rais wa Tanzania kama Kinara wa Uhamasishaji wa Masuala ya Wanawake na Vijana katika biashara na heshima iliyotolewa kwa Tanzania ya kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Wanawake na Vijana katika Biashara Eneo Huru la Biashara Barani Afrika.
Aidha, amesema mkutano huo ni muhimu sana kwakuwa umebeba agenda ya wanawake na vijana yenye lengo la kujenga haki na usawa wa kijinsia katika ajira, kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira, kuwajengea uwezo na kushirikishana uzoefu katika biashara na kuingia katika ushindani wa biashara kitaifa, kikanda na kimataifa.
