
Rais wa Urusi Vladimir Putin, amesema anaelewa kuwa China ina “maswali na wasiwasi” kuhusu vita vya Moscow nchini Ukraine, na kusifia uhusiano kati ya nchi yake na Taifa hilo.
Putin amesema hayo jana Alhamisi alipofanya mazungumzo na kiongozi wa China Xi Jinping nchini Uzbekistan.
Hadharani, China imechukua msimamo wa kutoegemea upande wowote kuhusiana na uvamizi wa Urusi ambao umeendelea kwa miezi 7, ingawa Rais Xi amesema moja ya kanuni kuu za sera ya nje ya Beijing, ni kwamba nchi zinapaswa kuheshimu mipaka ya mataifa mengine.
Katika kauli iliyopeperushwa kupitia televisheni mwanzoni mwa mazungumzo yao huko Samarkand, Putin alimwambia Xi, “Tunathamini sana msimamo wa usawa wa marafiki zetu wa China, kuhusu mzozo wa Ukraine.
“Tunaelewa maswali na wasiwasi wako kuhusu suala hili, na wakati wa mkutano wa leo, bila shaka tutafafanua haya yote kwa undani.
Matamshi ya Putin yalikuja wakati Ukraine, katika siku za hivi karibuni, imefanikiwa kutwaa tena maeneo makubwa, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo, ambayo Urusi ilikuwa imeteka katika wiki za mwanzo za vita.
Putin aliishutumu Marekani kwa msimamo wake kuhusu Taiwan na kukemea kile alichokiita ubabe wa Marekani na “azma ya kuutawala ulimwengu” na kusema kwamba anaona Urusi na China, zikishirikiana dhidi yake.
