Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, leo Ijumaa anakutana na rais wa Marekani, Joe Biden, White House, ambapo masuala ya biashara, nishati na usalama yakiwa ni agenda kuu.
Kile ambacho hakipo katika program rasmi, lakini kuna uwezekano wa kujadiliwa wachambuzi wanasema ni kuhusu masuala ya kidemokrasia na tofauti kuhusu uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.
Ziara ya kwanza ya Ramaphosa kwenda White House inafanyika wakati utawala wa rais Biden, unatafuta namna ya kushirikiana tena na Afrika ikichochewa na ziara ya karibuni ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Antony Blinken, barani Afrika ambapo alizindua mkakati mpya wa Washington kwa Afrika.
Wakati wa ziara yake ya Agosti, waziri Blinken alisisitiza kwamba Marekani inaichukulia Afrika kama mshirika mwenye hadhi sawa.
Hata hivyo, katika mkutano wao wa Pretoria, waziri wa mambo ya nje wa Afrika Kusini, Naledi Pandor, aliyashutumu mataifa ya magharibi kwa kuionea Afrika katika kuyataka mataifa yake kukemea uvamizi uliofanyika Ukraine.
Bob Wekesa ni mkurugenzi wa kituo cha Afrika kwa masomo ya Marekani katika chuo kikuu cha Witwatersrand, anasema.
“Katika mkutano ilikuwa wazi kabisa kwamba Afrika Kusini na Marekani zilikuwa katika njia mbili tofauti kuhusiana na masuala mengi.
Anasema kuna uwezekano Ukraine ikajitokeza tena wakati wa rais Biden na Ramaphosa watakapo kutana na ubashiri ni kwamba viongozi hao wawili watakuwa na mjadala mgumu wa masuala mbali mbali.
“Marekani kuchukuwa msimamo wa wazi kuiunga mkono Ukraine na kama kutaka kuwaondoa wanajeshi wa Urusi, Ukraine, itakuwa inajaribu kuishawishi Afrika Kusini ingawa itakuwa vigumu kubadilisha msimamo.
Afrika Kusini haikushiriki kupiga kura Umoja wa Mataifa mapema mwaka huu kushutumu uvamizi wa Urusi.
Baadaye rais Biden, alimpigia simu rais Ramaphosa. Taarifa ya baadaye ya White House baada ya simu hiyo ilieleza rais Biden alisisitiza umuhimu wa kuwa wazi, na mwitikio wa pamoja wa kimataifa dhidi ya uchokozi wa Urusi kwa Ukraine.
Steven Gruzd, mkuu wa programu ya utawala na diplomasia katika taasisi ya masuala ya kimataifa wa Afrika, amesema rais Ramaphosa na rais Biden watajadili masuala mengine, lakini nyongeza ya Ukraine haiwezi kuepukika.
“Katika agenda itakuwa biashara na uwekezaji, masuala kama mabadiliko ya hali ya hewa, hali ya chakula, amani na usalama katika Afrika yatajadiliwa, lakini yale yasiyo rasmi itakuwa ni vita vya Ukraine na mitazamo tofauti kati Afrika Kusini na Urusi na hasa mgogoro wenyewe,” amesema.
Gruzd ameongeza kuwa anatarajia musuada ya kukabiliana na shughuli za Urusi, barani Afrika, ambao umepitishwa na baraza la wawakilishi la Marekani na sasa ukisubiri kupitishwa na baraza la Seneti, utajitokeza katika mazungumzo ya viongozi hao wawili.
Mataifa ya Afrika yanaona muswada huo utaweka vikwazo kwa mataifa yanayofanya biashara na Urusi ikiwa ni jaribio la kuyaadhibu kwa kutopiga kura pamoja na Marekani kuhusiana na suala la Ukraine.
Mwezi Desemba, rais Biden anatarajia kuwa mwenyeji wa mkutano na viongozi wa Afrika mjini Washington.
