
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inathamini mchango wa mashirika ya serikali na binafsi katika Maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi.
Hemed ameyasema hayo hayo katika Hafla ya Uchangiaji Rasilimali za Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 iliyofanyika mapema wiki hii katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil, Kikwajuni Zanzibar.
Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kutambua umuhimu wa Mashirika hayo imeyashirikisha moja kwa moja katika suala la uchangiaji rasilimali za kufanikisha mchakato huo muhimu kwa taifa.
Hemed ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa ya Watu na Makazi, amesema uhitaji wa vifaa na rasilimali fedha Jumuiya ya Wafanyabiashara, asasi za kiraia na wadau wengine wamekuwa mstari wa mbele kuiunga mkono Serikali kwa kuleta mchango mzuri katika utekelezaji wake.
Aidha, ametumia fursa hiyo kuwapongeza Jumuiya ya Wafanyabiashara, mashirika ya serikali na binafsi kwa kuchangia rasilimali mbali mbali ili kufanikisha utekelezaji wa mchakato huo.
Sanjari na hilo Hemed amesema mchakato wa Sensa wa Watu na Makazi una umuhimu mkubwa kwani unaiwezesha Serikali na wadau mbali mbali kupata hesabu halisi ya idadi ya watu nchini pamoja na taarifa zao za kijamii, kiuchumi na makazi yao.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi Ya Makamu wa Pili wa Rais Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Hamza Hassan Juma amesema uelewa wa wananchi kuhusu Sensa ni mkubwa kutokana na uhamasishaji uliofanywa tangu mwanzo wa Mwaka huu.
Kwa upande wake Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Salum Kassim Ali amesema Serikali zote mbili zipo katika hatua za mwisho kukamilisha maandalizi ya Sensa ya watu na makazi Mwaka huu.
