
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, amesema Chama chake kinafuatilia kwa karibu utekelezaji wa mikakati ya kuwakwamua vijana dhidi ya umasikini.
Hivyo, Shaka amewataka watumishi wa umma kutafsiri kwa vitendo juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan za kuwatengenezea vijana fursa za kujikwamua kiuchumi.
Ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ifuta, kata ya Ukondamoyo, wilaya ya Urambo, mkoa wa Tabora, alipokagua ujenzi wa kituo cha afya Ifuta.
Amesema Rais ameonesha njia ya kwa kushusha fedha nyingi katika Halmashauri za wilaya kwa ajili ya kujenga au kuanzishwa miradi ya maendeleo.
“Tuliahidi ajira milioni nane katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa vijana na wanawake hadi ifikapo mwaka 2025.
“Kazi kubwa anayoifanya Rais Samia ni kutumia fedha za ndani kutengeneza fursa za ajira ili wananchi wajikwamue kiuchumi.
“Ni jukumu la watendaji wa serikali kutafsi kwa vitendo ili lengo hilo litimie na wananchi hususan vijana na wanawake wakwamuliwe kiuchumi,” amesema.
Shaka ameongeza kuwa CCM itaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa mkakati wa serikali ili ahadi ya Chama kupitia ilani ya uchaguzi itekelezwe na kufikia malengo.
Aidha, amesema katika kuwakwamua vijana, CCM haitatazama Itikadi bali inataka kuona fursa zinapatikana na wote wananufaika nazo.
