Kenya's Deputy President, William Ruto, delivers a speech during the memorial service for former Kenyan President Mwai Kibaki at the Nyayo National Stadium in Nairobi on April 29, 2022. (Photo by TONY KARUMBA / AFP) (Photo by TONY KARUMBA/AFP via Getty Images)

Salamu za pongezi zimetolewa kwa rais mteule wa Kenya William Ruto ambaye ametangazwa mshindi wa kinyan’anyiro kilichokuwa na ushindani mkali.
Rais Emmerson Mnagagwa alikuwa wa Zimbabwe amekuwa kati ya viongozi wa kwanza kutuma salamu za pongezi kwa rais huyo mteule.
Rais wa Somalia na Waziri mkuu wa Ethiopia pia walituma salamu za heri.
Ruto amechaguliwa kama rais wa tano wa nchi hiyo, baada ya siku sita za uhakiki wa kura, mchakato ambao ulisababisha hali ya taharuki na rabsha za hapa na pale.
Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi na mipaka, IEBC, Wafula Chebukati alimtangaza mshindi jana Jumatatu jioni katika ukumbi wa Bomas of Kenya, nje kidogo ya mji mkuu, Nairobi.
Ruto alipata kura milioni 7,176, 141 ambayo ni asili mia 50.49 ya kura zote zilizopigwa dhidi ya mpinzani wake wa karibu, mwanasiasa mkongwe, Raila Odinga aliyepata kura milioni 6,942,930, sawa na asili mia 48.85 ya kura zote.
Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Ruto alimshukuru Odinga kwa”kuendesha kampeni tulivu ya kunadi sera.”
“Hakuna aliyeshindwa katika uchaguzi huu. Nitawatumikia Wakenya wote,” Ruto aliwaambia waliohudhuria hafla hiyo, ambayo ilisusiwa na mpinzani wake wa karibu.
Awali hali ya wasiwasi ilitanda kwenye ukumbi huo pale ilipodhihirika kwamba Odinga hangehudhuria hafla hiyo, baada ya mawakala wake kusema kulikuwa na dosari katika uhakiki wa kura.
Hayo yalijiri huku baadhi ya makamishna wakiitisha kikao na waandishi wa habari na kusema kwamba hawakukubaliana na jinsi uhakiki huo ulivyofanyika.
