Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametangaza baraza jipya la mawaziri lenye jumla ya mawaziri 27 katika mabadiliko makubwa ya uongozi wa serikali, hatua inayochukuliwa kama sehemu ya kurekebisha utendaji na kuongeza ufanisi ndani ya serikali ya awamu ya sita.
Akizungumza katika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma, Rais Samia amesema mabadiliko hayo yanahusisha kuanzishwa kwa wizara mpya, kubadilishwa kwa baadhi ya wizara za zamani na kuingizwa kwa sura mpya serikalini.
Miongoni mwa walioteuliwa kwa mara ya kwanza ni Wanu Ameir, ambaye ni Naibu Waziri mpya wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, na Paul Makonda, Mbunge wa Arusha Mjini, aliyechaguliwa kuwa mmoja wa manaibu mawaziri katika Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo.
Rais Samia pia amewarejesha mawaziri kadhaa waliokuwa serikalini akiwemo Profesa Adolph Mkenda, Jumaa Aweso, Profesa Makame Mbarawa na Profesa Paramagamba Kabudi. Hata hivyo, baadhi ya mawaziri maarufu kama Hussein Bashe, aliyekuwa akiongoza Wizara ya Kilimo, hawakurejea katika baraza jipya.
Dotto Biteko, aliyekuwa Naibu Waziri Mkuu ameachwa kama ilivyo kwa Waziri wa muda mrefu Jenista Mhagama (Afya), Damas Ndumbaro (Katiba na Sheria), Suleiman Jaffo (Vwanda na Biashara) na Pindi Chana (Maliasili na Utalii).
