
Dhoruba kali ya mchanga imeukumba kwa mara nyingine tena mji mkuu wa Iraq, Baghdad na kusababisha vifo vya watu saba katika nchi jirani ya Syria.
Shirika la haki za binadamu la Syria limesema miongoni mwa waliopoteza maisha wamo watoto wawili.
Dhoruba hiyo iliyoambatana na upepo mkali, imeng’oa miti na kusababisha umeme kukatika katika jimbo la Deir al Zour.
Nchini Iraq, mamia ya watu walipata tatizo la kupumua.
Wizara ya afya nchini humo imekadiria kuwa takribani wagonjwa 2,000 wametibiwa kwenye hospitali mbalimbali kutokana na tatizo hilo.
Shirika la habari la Iraq INA limeripoti kwamba magari ya wagonjwa yamesambazwa kote nchini kusaidia watu walio katika hatari ya kukosa hewa.
Mei 5, 2022, watu wapatao 5,000 walikutwa na tatizo la kupumua lililotokana na kimbunga cha mchanga katika maeneo mbalimbali ya Iraq.
