
Wabunge wa Sweden na Finland wamefanya mjadala kuhusu nchi zao kujiunga na mfungamano wa kijeshi wa Nato ili kujihami dhidi ya Urusi.
Finland ilitangaza rasmi jana uamuzi wa kuomba uanachama katika mfungamano huo.
Na nchini Sweden chama tawala kinaunga mkono wazo hilo na hivyo kutayarisha njia ya kuwa mwanachama hatua ambayo inawakilisha mabadiliko ya sera za nchi hizo.
Finland imekuwa inaendesha sera ya kutofungamana na upande wowote kwa muda wa miaka zaidi ya 75 wakati Sweden imeendesha sera hiyo kwa muda wa karne mbili.
Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema uamuzi wa Nato wa kujitandaza unaweza kusababisha jibu kutoka Urusi.
Hata hivyo, waziri mkuu wa Finland Sanna Marin ameeleza kuwa mazingira ya kiusalama ya nchi yake yamebadilika kimsingi.
Amesema nchi inayohatarisha usalama wa bara la Ulaya ni Urusi ambayo kwa sasa inaendesha vita vya kivamizi.
