
Jamii imehimizwa kupenda kula machungwa kwa kuwa ni miongoni mwa matunda yenye utajiri mkubwa wa vitamini C.
Mtaalamu wa virutubisho tiba, Abdallah Mandai ameyasema hayo leo Mei 26, 2022, jijini Dar es Salaam, kama ilivyo desturi yake ya kutoa mada mbalimbali kwa jamii zinazohusu kulinda na kuimarisha afya zao.
“Chungwa ni tunda tamu na lenye rangi ya kuvutia pia. Kama yalivyo matunda mengine, linapendwa na kuliwa na watu wa rika na jinsia zote.
“Chungwa limesheheni kambalishe (fibre) ambazo zina umuhimu mkubwa wakati wa tendo la usanisi wa chakula tumboni, pamoja na mambo mengine lina uwezo wa kupambana na aina mbalimbali za magonjwa.
“Kula chungwa kunasaidia kukata kwikwi, kung’arisha ngozi na kutibu vidonda vya nje. Pia ni tunda muhimu kwa wanaokabiliwa na maradhi ya kisukari, wale japo kipande kimoja cha chungwa kwa siku.
“Licha ya kusheheni vitamini C, chungwa pia lina virutubisho vya flavonoids na phytonutrients ambavyo vinasaidia kumwondolea mlaji hatari ya kupata magonjwa ya moyo.

“Vitamini C iliyomo katika chungwa inasaidia kukuepusha na maradhi ya vidonda vya tumbo na kama tayari unavyo itakusaidia kupata nafuu.
“Madini ya calcium yaliyomo kwenye chungwa yanasaidia kuimarisha mifupa ya meno, hivyo kula machungwa kwa wingi kunamwepusha mlaji na hatari ya kupata maradhi ya kiseyeye.
“Machungwa yana wingi wa vitamini B6 na madini ya chuma ambavyo vinasaidia kuzalisha seli hai nyekundu za damu zinazofanya kazi ya kusafirisha hewa safi (oksjeni) mwilini.
“Tunda hili limebainika kuwa na asilimia 10 ya asidi ya folic ambayo ni muhimu kwa afya ya ngozi na ukuaji wa ubongo pamoja na kuimarisha kumbukumbu.
“Wenye tatizo la mawe katika figo chungwa linasaidia kuyaondoa, kula tunda hili mara nyingi ili kupata faida zilizomo.
“Chungwa pia limesheheni virutubisho vya magnesium na hesperidin ambavyo vinasaidia kuondoa tatizo la shinikizo la juu la damu.
“Kutokana na faida hizo machungwa ni vema yatumiwe kwa wingi na wagonjwa wenye tatizo hilo,” amesema.
Mtaalamu huyo ameendelea kusema “Huwezi kumaliza kutaja shehena ya faida za chungwa ila itoshe tu kusema kuwa tunda hili ni kinga na dawa hivyo tujitahidi kulitumia kila siku kulinda na kuimarisha afya zetu.
