Zaidi ya watu 50 wameuawa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo baada ya waasi wa kundi la ADF kuwashambulia kwa mapanga wakati wa mazishi.
Afisa wa serikali katika eneo hilo Macaire Sivikunula ameziambia duru za habari kwamba, shambulio hilo limetokea katika kijiji cha Ntoyo, kilichopo katika eneo la Lubero, jimbo la Kivu Kaskazini.
Msimamizi wa kijeshi wa Lubero Kanali Alain Kiwewa, ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba, idadi ya watu waliouawa ni takriban watu 60 na huenda ikaongezeka kwani baadhi ya watu bado hawajapatikana.
Jeshi la serikali ya Kongo kwa kushirikiana na Uganda, limeeleza kwamba limeimarisha operesheni ya kijeshi dhidi ya kundi la waasi wa ADF wa Uganda katika wiki za hivi karibuni.
Mwezi uliopita, kundi la ADF liliwaua zaidi ya watu 50 huku likiwaua watu wengine 38 katika shambulio tofauti la kanisa mnamo mwezi Julai.
Wakati jamii inajaribu kuelewa athari za mauaji haya ya halaiki, shinikizo linaongezeka kwa serikali ya Congo kuchukua hatua madhubuti na za kudumu kukabiliana na tishio la ADF mashariki mwa taifa hilo.
Waasi wa ADF ambao asili yao wanatokea Uganda, wamekuwepo kaskazini mashariki mwa DRC tangu katikati ya miaka ya 1990, ambako wapiganaji wake wameua maelfu ya raia. Mwishoni mwa 2021, Uganda na DRC zilianzisha operesheni ya pamoja ya kijeshi dhidi ya waasi hao.
Hata hivyo, operesheni hiyo iliyopewea jina la “Shujaa”, haijafanikiwa hadi sasa kukomesha mashambulizi ya kundi hilo.
