Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, ameelekeza mambo matatu kwa viongozi wa chama ili kufanikisha ushindi wa kishindo kwa mgombea Urais, Dk. Samia Suluhu Hassan, pamoja na wagombea ubunge na udiwani.
Ameyataja mambo hayo kuwa ni kuvunja makundi, kueleza mambo makubwa na mazuri yaliyotekelezwa kupitia Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa kipindi cha miaka minne, pamoja na kuwahamasisha wananchi kujitokeza kupiga kura na kuwapigia wagombea wa CCM.
Wasira aliyasema hayo leo mjini Morogoro alipokutana na viongozi wa CCM, wakiwemo mabalozi na wenyeviti wa mashina, katika siku ya kwanza ya ziara yake mkoani humo.
“Kwa hiyo ndugu zangu, baada ya kuwaeleza hayo, nataka niwakumbushe kuvunja makundi na kutangaza kazi zilizofanywa katika miaka minne ya utendaji wa mgombea wetu wa urais, Dk. Samia Suluhu Hassan.
“Ili watu wapige kura, ni lazima sisi viongozi tuwahamasishe kwenda kupiga kura. Maana wapo wengine, hata wanachama wetu, wanasema: ‘Si ameshapita Aboud? Basi tumemaliza.’ Wanafikiri kura ya maoni ndiyo inaweka mbunge.
“Kura ya maoni haimfanyi mtu kuwa mbunge. Ndiyo maana Aboud tunamwita mbunge mteule wa ndani ya CCM, kwa sababu wa nje watakuja kushindana naye,” alisema.
Aliongeza: “Sasa sisi kazi yetu ni kuhakikisha watu wanajitokeza na tunawashawishi kwa nini waipigie kura CCM. Kazi nyingine ni kuwaambia waende wakapige kura.”
Wasira alisema mabalozi wa nyumba 10 ndiyo mhimili wa Chama, kwa kuwa Chama kinaanzia chini. Aliongeza kuwa mwaka huu mabalozi wote wamepewa usafiri kama nyenzo ya kufanikisha kazi hiyo.
“Kile ni kitendea kazi cha kwenda nyumba kwa nyumba kuwaambia wananchi: ‘Leo ni siku ya kupiga kura, tokeni nyote mkapige kura.’
“Katika mfumo wa zamani, ukikosa mpinzani ulikuwa unapita bila kupingwa. Lakini sasa, kwa mfano, tunapokuwa na mgombea wetu na wapinzani hawajitokezi, hali hiyo inahitaji nguvu zaidi. Watu wanaweza kufikiri tayari imemalizika, kumbe bado.
“Mgombea lazima ashinde kwa kura nyingi za ndiyo kuliko za hapana. Vilevile, Rais wa Jamhuri ya Muungano anahitaji kura nyingi kila mahali. Atazipata wapi kama watu hawajitokezi?”
