
Rais, Samia Suluhu Hassan, amewataka viongozi wa vyama vya siasa na wadau wa demokrasia ya vyama vingi nchini kuweka utaifa mbele ili kukuza maendeleo na demokrasia.
Mama Samia ametoa kauli hiyo leo Aprili 5, 2022, jijini Dodoma wakati akihutubia kwenye Mkutano wa Kitaifa wa Maridhiano, Haki na Amani ulioandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD).
Katika mkutano huo, Rais Samia amewataka viongozi wote wa vyama vya siasa pamoja na wadau wa demokrasia ya vyama vingi kuweka utaifa mbele na kushiriki katika kukuza maendeleo na demokrasia nchini.
Amesema viongozi wanaoongea kuhusu haki lazima watambue kuwa haki ni ya pande zote mbili na kwamba kila mmoja ana wajibu wa kutambua kuwa inapoishia haki yake basi inaanza haki ya mtu mwingine.
Rais Samia ameahidi kushirikiana na wadau wa haki za binadamu na kusisitiza kuwa ushirikiano kutoka serikalini ni wa uhakika na kwamba serikali ina dhamira ya dhati ya kushirikiana na Watanzania kutengeneza Tanzania ya kweli.
Katika mkutano huo, Rais Samia amegusia baadhi ya mambo yaliyoainishwa katika mapendekezo ya rasimu ya Katiba ambapo anategemea kupokea mapendekezo yanayotekelezeka ili iwe rahisi kwa serikali kuyatekeleza lakini si kwa yale yasiyotekelezeka.
Kwa upande mwingine, mwenyekiti wa kituo hicho anayemaliza muda wake, Zitto Kabwe ametoa shukrani kwa Rais Samia kuhudhuria mkutano huo lakini pia ameiomba serikali yake ikipatie fedha za ruzuku kituo hicho ambacho kinategemea fedha za misaada katika bajeti ya uendeshaji.
Mwenyekiti wa sasa wa kituo hicho Zitto Kabwe anamaliza muda wake wa utumishi na anamkabidhi Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana.
