
Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Nchini (TMDA), imesema matumizi ya tumbaku yanaweza kusababisha matatizo kwenye via vya uzazi na kansa ya utumbo mpana.
Hivyo, imetoa mwito kwa wananchi kuacha kutumia tumbaku na mazao yake ili kuepukana na athari hizo nyingine.
Ofisa Mwandamizi wa Elimu kwa Umma na Huduma kwa wateja, Roberta Feruzi, ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari eneo la Mwahako jijini Tanga, ambako kunakofanyika maonesho ya 9 ya viwanda, biashara na utalii.
Amesema TMDA imeshiriki maonesho hayo ili kutoa elimu kwa wananchi kwa kuwa imepewa dhamana ya kusimamia na kudhibiti bidhaa za tumbaku. “Lakini kubwa ni kundi la vijana wenye umri wa chini ya miaka 18, wao wamekuwa wakijiingiza kwenye uvutaji, nanatoa mwito waache mara moja kwani madhara yake ni makubwa,” amesema.
Hata hivyo, amesema wameshiriki kwenye maonesho hayo kwa ajili ya kutoa elimu kwa wananchi waifahamu taasisi hiyo na kazi zake.
“Lakini pia tunasimamia udhibiti wa bidhaa zinazotokana na tumbaku,TMDA tunahakikisha jamii na wanaotoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya dawa wengi wamekuwa wakikiuka kanuni,” amesema
