
Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani, Elisha Osati amesema licha ya kuonekana hali ya kutulia nchini kwa sasa ugonjwa wa corona bado upo.
Dk. Osati amesema takwimu ambazo zimekuwa zikitolewa na Wizara ya Afya zinaonesha ugonjwa bado upo miongoni mwa jamii na katika hospitali mbalimbali hapa nchini zinawagonjwa wa corona.
Ametoa kauli hiyo hivi karibuni wakati wa kampeni ya kuhamasisha uchanjaji wa chanjo ya UVIKO19 inayotekelezwa na Amref Health Africa Tanzania.
Dk.Osati amefafanua kuwa kwa sasa takriban asilimia 98 ya wagonjwa wote wanapokelewa hospitalini ni wale ambao hawajachanjwa hali inayoonesha kuwa waliochanjwa wameendelea kuwa salama zaidi dhidi ya corona.
“Tungeendelea kuona nchi nyingine duniani zikipambana na ugonjwa huu kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwamo kuchanja chanjo imebaki kuwa moja kati ya mbinu ambazo zimeonesha matokeo mazuri hasa kwenye kupunguza wagonjwa pamoja na kasi ya kusambaza kwa ugonjwa huu hatari na Korona,”amesema.
Ametoa mwito kwa Watanzania kutopuuzia suala la chanjo wakati taifa linapopambana kutokomeza ugonjwa hua ndani ya nchi yetu.
Amesisitiza kuwa chanjo zinazotolewa hapa nchini katika hospitali zote pamoja na vituo maalumu ni salama na kinga yake inaweza kusaidia hata pale ambapo kirusi kinaweza kujibadilisha na kuja katika mfumo mpya.
Amref Health Africa Tanzania wameendelea kuwa mstari wa mbele kufikisha elimu kwa Watanzania kuhusu ugonjwa huo hatari na namna ambavyo watu wanaweza kujikinga ili wabaki salama wao na wapendwa wao.
