
Tanzania imeendelea kutoa mwito wa kuiondolea Zimbabwe vikwazo vya kiuchumi vinavyodumaza jitihada za nchi hiyo kujiletea maendeleo.
Mwito huo umetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula, wakati wa Mkutano wa majadiliano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Umoja wa Ulaya (EU) uliofanyika kwa njia ya mtandao jana Juni 16.
Balozi Mulamula amesema hakuna sababu ya kuendelea kuiwekea vikwazo Zimbabwe ilihali imefanya mabadiliko ya kimfumo katika maeneo mengi yakiwamo ya siasa, uchumi na mifumo ya sheria.
Akijibu hoja hiyo, EU kupitia Waziri wa Mambo ya Nje wa Ureno, Augusto Santos Silva imesisitiza umuhimu wa Zimbabwe kuendelea kufanya mabadiliko katika mifumo yake na kudai kuwa vikwazo vilivyosalia havina athari kwa watu wa Zimbabwe.
Amesema licha ya vikwazo hivyo, EU imeendelea kushirikiana na Zimbabwe kwa kuipatia misaada ya maendeleo na ya kibinadamu ambapo Euro milioni 366 na milioni 66 mutawalia zimetolewa kwa Zimbabwe katika kipindi cha miaka saba iliyopita.
Katika majadiliano hayo yenye lengo la kusaidia kukuza uchumi na maendeleo katika kanda ya SADC, Mawaziri hao walijadili kuhusu janga la UVIKO-19 na athari zake katika ukuaji wa uchumi na mikakati ya kujikwamua kiuchumi baada ya ugonjwa huo kudhibitiwa. Umoja wa Ulaya umeahidi kuendelea kushirikiana na nchi za SADC kupitia programu mbalimbali zikiwamo za kuhakikisha kila mtu anapata chanjo na programu nyingine nafuu kama kulipa madeni na misaada ya fedha za kukabiliana na athari za UVIKO-19.
Kuhusu mikakati ya kukabiliana na UVIKO-19, Nchi za SADC kupitia Waziri wa Mambo ya Nje wa Msumbiji, VerĂ³nica Macamo alizihimiza nchi za EU kuzijengea uwezo nchi za SADC kwa kutengeneza vifaa vya kukabiliana na UVIKO-19 badala ya kuagiza vifaa hivyo kutoka nchi zilizoendelea.
