
Waziri wa Fedha na Mipango, Dakta Mwigulu Nchemba, amesema wananchi wametafsiri kinyume na lengo la Serikali baadhi ya tozo alizowasilisha bungeni wakati wa mapendekezo ya Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2021/22.
Dakta Nchemba ametoa ufafanuzi huo jijini Dodoma alipokutana na kuzungumza na Wahariri wa vyombo vya habari nchini kupitia Jukwaa la Wahariri (TEF), katika kikao kilichoandaliwa na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Amesema kodi hizo zimetafsiriwa kinyume na lengo la Serikali, ambapo kwenye kodi ya kuongeza salio mtu akiweka kuanzia Sh. 1000 hadi Sh. 2500, atatozwa shilingi 10, shilingi 2500 hadi 5000 atatozwa Sh. 21, shilingi 50,000 hadi 100,000 atatozwa shilingi 186 na shilingi 100,000 kwenda juu anatozwa shilingi 200 na sio kila siku ni pale anapoweka muda wa maongezi.
Amesema baadhi ya watu wamezua mkanganyiko kuwa serikali imeweka kodi kwenye laini za simu kama ambavyo baadhi ya wananchi na wabunge wamekuwa wakichanganya.
Amebainisha kuwa haimaanishi kwamba shilingi 10 sio mzigo lakini Serikali iliangalia matatizo yaliyopo na kugundua kuwa yanagharimu zaidi, kuliko thamani ya shilingi 10 itakayotozwa kama kodi.
Amefafanua kuwa miradi mikubwa inayotekelezwa nchini ukiwamo wa mradi wa Bwawa la umeme la Mwalimu Nyerere unahitaji zaidi ya shilingi trilioni 4 na ujenzi wa Reli ya Kisasa unaohitaji zaidi ya shilingi trilioni 20 hadi kukamilika.
Dakta Mwigulu amesema iwapo fedha zote zitategemea mikopo nchi itapitiliza uwezo wa kukopa na kutokukopesheka hivyo ushiriki wa wananchi ni muhimu.
