
Rais mteule William Ruto leo Jumatano, Septemba 7, amefichua maelezo ya mazungumzo yake ya simu na Rais Uhuru Kenyatta.
Katika taarifa, Ruto amebainisha kuwa walijadili kura iliyohitimishwa ya Agosti 9 na mchakato wa mpito kama ilivyoainishwa katika Katiba.
“Nilifanya mazungumzo ya simu na bosi wangu, Rais Uhuru Kenyatta. “Tulijadili Uchaguzi Mkuu uliomalizika hivi punde na mpito kama inavyotarajiwa na mila na desturi zetu za kidemokrasia,” amesema.
Uhusiano kati ya wawili hao uliharibika baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuamua kumuunga mkono Raila Odinga katika kinyanganyiro cha Uchaguzi wa Urais 2022.
Wakati wa kampeni za uchaguzi huo wawili hao walirushiana cheche za maneno hadharani kuthibitisha uhusiano mbaya kati yao.
Na hata baada ya William Ruto kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa mwaka huu na kuvutia pongezi kutoka viongozi wa maeneo mbalimbali, imedaiwa kwamba Uhuru Kenyatta hajampongeza naibu wake.
