
Rais Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kwa mkuu wa mkoa wa Mtwara, Brigedia Jenerali Marco Elisha Gaguti, kufuatia vifo vya watu 14 waliofariki dunia katika ajali ya barabarani.
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Jaffar Haniu, katika taarifa yake vya vyombo vya habari aliyotoa leo, amesema ajali hiyo imetokea jana Januari 02, 2022, saa 2:15 usiku katika kijiji cha Lidumbe, wilaya ya Newala, mkoani humo.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Mtwara, ACP Mark Njera amesema chanzo cha ajali hiyo iliyotokea katika barabara ya ‘Uchumi’ Mtwara-Tandahimba-Newala-Masasi ni mwendokasi wa dereva wa gari aina ya Scania wakati aliposhindwa kulimudu na kwenda kuwagonga watu hao hali iliyopelekea vifo hivyo na kujeruhi wengine 22.
Rais Samia amemtaka Brigedia Jenerali Gaguti kufikisha salamu zake za pole kwa wafiwa wote, ndugu, jamaa, marafiki na anaungana na familia hizo katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.
Mama Samia pia amewaombea kwa Mwenyezi Mungu roho za marehemu wote mahali pema peponi, amina.
Aidha, Rais Samia amevitaka vyombo vyote vinavyosimamia usalama barabarani kuongeza juhudi za kudhibiti ajali hasa katika kipindi hiki cha mwanzo wa mwaka, na pia amewaasa madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani.
