
Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari amewahimiza wanaowania tikiti ya chama tawala katika nafasi ya uraisi kuafikiana kabla ya kura ya mchujo wiki hii.
Chama tawala cha All Progressives Congress (APC), kitafanya mkutano wake kuanzia leo Jumatatu hadi Jumatano kumchagua mshika bendera katika kuwania urais.
Wagombea 13 wameruhiswa kugombea wadhfa huo. Rais Buhari amewataka wagombea hao kufanya mashauriano kati yao ili kupunguza idadi ya wagombea, kuleta mgombeaji mwenye ushawishi na kupunguza wasiwasi miongoni mwa wanachama.
Buhari hajaidhinisha mgombea yeyote na yeyote atakayeibuka kinara wa chama cha APC atakabiliana na mpinzani mkuu wa upinzani, makamu wa rais wa zamani Atiku Abubakar wa People’s Democratic Party (PDP), pamoja na wagombea kutoka vyama vingine.
