
Watu 13 wameuawa na wengine 21 kujeruhiwa baada ya mshambuliaji kuvamia shule moja katika mji wa katikati ya Urusi wa Izhevsk.
Gavana wa jimbo hilo amesema bado hawajamjua aliyefanya mashambulizi hayo.
Kikosi cha Uchunguzi cha Urusi kimesema miongoni mwa watu 13 waliouawa, saba walikuwa watoto na 6 watu wazima ambao ni pamoja na walimu na walinzi.
Kikosi hicho kimesema mshambuliaji ambaye mwili wake umekutwa ndani ya shule hiyo, alikuwa mwanamme aliyevalia fulana yenye alama za Kinazi.
Msemaji wa Ikulu ya Kremlin, Dmitry Peskov, ameyaita mashambulizi hayo kuwa ni ya kigaidi na aliwaambia waandishi wa habari kwamba Rais Putin amehuzunishwa sana na vifo hivyo na anaungana na ndugu na jamaa waliouawa na majeruhi.
