
Mchungaji kiongozi, Wilson Jacob wa Kanisa la Pentecost Kisarawe (KLPK) MMPT amesema watu wasio na idadi wameshuhudia jinsi walivyomwona Mungu ndani ya kanisa lisilofungwa tangu kujengwa kwake miaka 25 iliyopita.
Ameyasema hayo hivi karibuni wakati akizungumza na lililotembelea katika kanisa hilo lililoko pembezoni mwa barabara kuu ya kutoka Dar es Salaam kuingia mji wa Kisarawe.
Mchungaji Jacob amesema watu wa imani tofauti wamekuwa wakiingia ndani ya kanisa hilo wazi kuomba shida zao mbalimbali na kumwona Mungu akijibu haja zao.
“Mtu ana kesi mahakamani anakuja hapa anaomba anaondoka zake, mwingine anakuja hospitali anapita hapa anaomba anaondoka zake, tunapata shuhuda nyingi sana kutoka kwa wapita njia.
“Wanaouguza wagonjwa wao wanakuja hapa kukesha, wengine wanasafiri hawana pa kulala wanalala hapa, wengine wanakuja kuomba msaada wa kuhifadhi wafu wao tunawapatia,” amesema Mchungaji huo.
Amefafanua kuwa watu wanaoomba hifadhi ya kulala hapo ni wa Imani tofauti, pamoja na wasio Wakristo.
Akifafanua kwanini nyumba hiyo ya ibada inabaki wazi tena bila mlinzi amesema tangu jengo hilo linaanza kujengwa kwa msaada wa raia wa Sweden nao walishauri libaki wazi kutoa fursa kwa watu wanamtafuta Mungu kuingia muda wowote.
“Zaburi ya 26 inasema Bwana asipoulinda mji kila aulindaye anafanya kazi bure, hata tukiweka walinzi mchana na usiku bado watafanyakazi bure.
“Tunaamini mlinzi mkuu ni Mungu, tunaliacha wazi kuwapa fursa watu mbalimbali wanaotaka kushinda au kusali humu wafanye hivyo,” amesema Mchungaji Jacob.
Akizungumzia namna jengo hilo lilivyojengwa na kuliwekea imani kwa Mungu ya kulilinda amesema”Imani inafanyakazi kutokana na kiwango mtu anachoamini, imani haina fotokopi, hivyo kila watu wanatumia msingi wa jengo lao kutokana na imani yao kwa Mungu, tangu mwanzo tuliweka imani kwa Mungu.
Kanisa hilo ambalo makao yake makuu Kijitonyama Pentecost Church jijini Dar es Salaam, ni miongoni mwa makanisa yaliyochochea imani miongoni mwa jamii ya wana-Kisarawe kubadilisha maisha ya wengi kiimani.
