
Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis, yupo nchini Canada kwa ziara ya wiki nzima.
Ziara hiyo imejikita katika kuomba radhi kwa niaba ya Kanisa hilo, kutokana na udhalilishaji ambao watoto wa jamii ya watu wa asili walipitia kwa sehemu kubwa katika shule zinazosimamiwa na kanisa.
Papa Francis anatarajiwa kutembelea parokia moja mjini Maskwacis, ambako atafanya maombi kwenye eneo la makaburi, na baadaye atahutubia wawakilishi wa makundi ya jamii za watu wa asili, kabla ya kufanya mkutano mwingine mchana na watu wa jamii hiyo mjini Edmonton.
Kukutana na watu wa jamii ya asili ni sehemu muhimu ya ziara ya papa ya siku sita, baada ya ugunduzi wa miili ya watoto zaidi ya mwaka mmoja uliyopita, karibu na shule za bweni ambazo wakati moja ziliendeshwa na Kanisa Katoliki.
Ugunduzi huo ulitoa mwanga kuhusu ukatili waliofanyiwa watoto wa jamii za asili, waliotenganishwa na familia zao na kudhalilishwa na wafanyakazi wa shule. Jamii hizo zimemtaka Papa aombe msamaha kwao akiwa Canada.
