
Ili kunufaika na vitamini C, inayosaidia kuboresha kinga za mwili mtaalam wa virutubisho tiba, Abdallah Mandai ametoa mwito kwa jamii kutumia ukwaju.
Amesema vitamini nyingine B, E na, madini ya chuma, calcium, potassium, manganese, phosphorus na nyuzinyuzi ambazo zina umuhimu mkubwa katika kutatua matatizo ya maumivu ya mifupa na misuli zinapatikana pia katika ukwaju.
Mandai ameyasema hayo leo Julai 25, 2022 jijini Dar es Salaam, wakati akizungumzia vitamini na madini mbalimbali na kazi zake kwenye mwili wa binadamu.
“Vitamini nyingine muhimu zinazopatikana kwenye ukwaju ni B complex’ na ‘thiamine,’ ambazo ni miongoni mwa zile muhimu katika makundi ya vitamin, hizi zinafanya kazi ya kuboresha mifumo ya fahamu mwilini na kuufanya mwili uweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
“Penda kula ukwaju kama tunda au kunywa juisi yake, unasaidia kurekebisha na kuboresha mfumo wa mmeng’enyo wa chakula tumboni kwa kuwa umesheheni nyuzinyuzi lishe (fiber).
“Aidha, tafiti mbalimbali zimebaini unapokula ukwaju unakuwa katika uwezekano wa kuondokana na tatizo la kuharisha,” amesema Mtaalam huyo.
Aidha, amebainisha kuwa matatizo ya shinikizo la juu la damu nayo yanaweza kupata ahueni endapo mgonjwa atatumia ukwaju wenye utajiri wa madini ya ‘potassium’, ambayo yanafanya kazi ya kushusha msukumo wa damu mwilini.
Mandai ametanabahisha kuwa ukwaju pia una uwezo wa kuhakikisha usalama wa afya ya moyo wako kutokana na uwezo wake mkubwa wa kupunguza kiwango cha lehemu mwilini.
“Faida nyingine za tunda hili lina nafasi ya kuongeza mzunguko wa damu mwilini kutokana na kuwa na madini ya chuma ambayo yana nafasi ya kuongeza asilimia 10 ya mahitaji ya mzunguko wa damu mwilini kwa kila siku.
“Pia linasaidia uhakika wa hewa ya oxgeni kuenea vizuri mwilini hasa kwenye mifumo ya mwili inayohitaji hewa katika utendaji kazi wake,” amesema.
Aidha, amesema ukwaju unafaa kwa wenye shida ya kisukari kwa kuwa una uwezo wa kufyonza kabohydrate inapozidi mwilini ambayo inachangia matatizo makubwa kwa mtu anayesumbuliwa na kisukari.
“Si matunda ya ukwaju pekee ndiyo yenye faida bali hata mizizi yake, ina uwezo wa kutatua tatizo la maambukizi ya njia ya mkojo. Mizizi ya ukwaju pia ni msaada kwa kinamama wenye tatizo la uzazi ambao pia wanakabiliwa na maumivu ya tumbo wakati wa hedhi.
“Majani ya mkwaju yakikaushwa kivulini na kusagwa yachanganywe na mafuta ya nazi yanasaidia kuondoa shida mbalimbali za ngozi na maumivu ya miguu hasa inayokufa ganzi.
“Unga huo wa majani ya ukwaju, pia unasaida kutuliza tatizo la pumu, endapo utachanganywa na kiasi kidogo cha asali na mgonjwa kuulamba. Tetekuwanga ni miongoni mwa magonjwa yanayoweza kutibiwa kwa kutumia majani ya ukwaju pia,” amesema.
