
Jumuia ya Kujihami ya NATO, imeitaja Urusi kuwa tishio la moja kwa moja na kubwa kabisa kwa usalama wa nchi za Magharibi baada ya uvamizi wake nchini Ukraine.
NATO imekubaliana kuhusu mipango ya kuliboresha jeshi la Ukraine ikisema inasimama kikamilifu na Waukraine katika ulinzi wa kishujaa wa nchi yao.
Akizungumza mjini Madrid ambako kunafanyika mkutano wa kilele wa viongozi wa NATO, Katibu Mkuu Jens Stoltenberg amesema jumuia hiyo ilikubaliana kutoa msaada wa kifedha na kijeshi wa kipindi kirefu kwa ajili ya kuliboresha jeshi la Ukraine ambalo kwa sehemu kubwa ni la enzi ya Sovieti.
Rais Vladmir Putin amesema Urusi itajibu kwa kuchukua hatua kali kama NATO itaweka miundo mbinu nchini Finnland na Sweden baada ya nchi hizo kujiunga na muungano huo wa kijeshi unaoongozwa na Marekani.
