
Mkutano uliocheleweshwa kwa muda mrefu kuhusu kurejesha hali bora ya bahari zote ulimwenguni umeanza mjini Lisbon, Ureno.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema bahari zimo katika hali mbaya.
Guterres amewaambia wajumbe wanaohudhuria mkutano huo wa mjini Lisbon kwamba dunia inakabiliwa na hali ya hatari kwenye bahari.
Amesema bahari zimechafuka na zimeathiriwa na mabadilikio ya tabia nchi.
Katika hotuba yake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekumbusha kuwa bahari zinachangia hadi asilimi 50 ya hewa safi ambayo binadamu wanahitaji.
Naye mkuu wa kitengo cha mradi wa uchumi wa baharini kwenye benki ya dunia Charlotte de Fontaubert amesema sasa binadamu ndiyo wanatambua kiwango cha madhara yaliyotokea kwenye bahari ambayo yamesababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa.
Amesema hali inazidi kuwa mbaya kutokana na uchafu unaotupwa majini kila siku na hasa taka za plasitiki.
Kulingana na utafiti uchafu wa plastiki utaongezeka na kufikia tani karibu bilioni moja ifikapo mwaka 2060.
