Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ameagiza kurejeshwa kwa huduma ya mabasi ya mwendokasi katika kituo cha Mbagala kuanzia Alhamisi, Novemba 20, 2025, ikiwa ni sehemu ya hatua za awali za serikali kufuatia vurugu zilizojitokeza baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29.
Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua baadhi ya vituo vilivyoharibiwa katika Wilaya ya Temeke, Chalamila alisema serikali ina wajibu wa kuhakikisha wananchi wanapata huduma muhimu bila kuchelewa, hasa katika maeneo yaliyoathirika zaidi kama Mbagala.
Agizo hilo linakuja kufuatia ombi la Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda, ambaye aliomba baadhi ya huduma muhimu, zikiwemo za usafiri wa mwendokasi, kurejeshwa kwa haraka ili kupunguza usumbufu kwa wakazi wa eneo hilo.
Aidha, Chalamila ameeleza kuwa licha ya uharibifu mkubwa wa vituo vya mwendokasi, hakuna shule yoyote iliyoripotiwa kuchomwa au kuharibiwa.
Amesisitiza kuwa serikali itaendelea na tathmini ya uharibifu wa mali za umma na watu binafsi ili kuweka mkakati madhubuti wa urejeshaji wa huduma hizo.
Chalamila pia ametoa wito kwa wananchi wa Dar es Salaam kuwa watulivu na kudumisha amani, mshikamano na upendo miongoni mwao.
Amesema ni muhimu kwa jamii kutoangalia migogoro ya kisiasa kwa mtazamo wa juujuu, kwani inaweza kuchochea mgawanyiko wa kitaifa na kutoa mianya kwa maadui wa taifa kuivuruga amani.