
Viongozi wa Jumuia ya Afrika Mashariki wamekubaliana kutuma kikosi cha kikanda kukomesha mapigano Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Uamuzi huo umetangazwa na ofisi ya rais wa Kenya Uhuru Kenyatta baada ya viongozi wa nchi saba wanachama kufanya mazungumzo jijini Nairobi kuhusu ongezeko la machafuko mashariki mwa Kongo ambayo yamezinasa nchi jirani.
Taarifa ya ofisi ya Kenyatta imesema wakuu wa nchi wameagiza kikosi cha kikanda kinachotakiwa kwa ushirikiano na majeshi ya Kongo kuimarisha na kudumisha amani nchini Kongo.
Viongozi hao wametaka machafuko yasitishwe mara moja na usitishwaji wa mapigano uanze kutekelezwa.
Rais wa Kongo Felix Tshisekedi na rais wa Rwanda Paul Kagame walihudhuria mkutano huo ulioandaliwa na rais Kenyatta.
Marais wa Burundi, Sudan Kusini na Uganda pia walihudhuria huku Tanzania ikiwakilishwa na balozi wake mjini Nairobi.
