
Jeneza lenye mabaki ya mwili wa Patrice Lumumba shujaa wa uhuru wa Congo aliyeuawa limerejeshwa nchini mwake kwa ajili ya mazishi.
Mabaki ya Lumumba yaliwasili jana Jumatano ikiwa ni zaidi ya miongo sita baada ya kuuawa kwake.
Ndege ilichukua mabaki ya Lumumba, hasa jino ambalo mkoloni wa zamani wa Congo, Ubelgiji, alilikabidhi kwa familia yake Jumatatu wiki hii, kutoka Brussels Ubelgiji hadi Kinshasa.
Mabaki hayo yatapitishwa katika maeneo mbalimbali ya taifa hilo muda wa siku tisa.

Jeneza na wajumbe walioandamana nalo walisafiri kwa ndege hadi mkoa wa kati wa Sankuru, ambako kiongozi huyo wa kwanza wa nchi hiyo baada ya uhuru alizaliwa katika kijiji cha Onalua mwaka wa 1925.
“Mheshimiwa waziri mkuu wangu wa kwanza, polisi na wanajeshi wa DRC wamejipanga kukupa heshima zao ukirejea kijijini mwako,” ofisa wa polisi aliyesimama kwa umakini amesema, mbele ya jeneza lilipowasili kwenye uwanja wa ndege katika mji wa Tshumbe.
Kutoka hapo, lilipelekwa kilomita 25 hadi Onalua, ambako siku mbili za kutoa heshima zimepangwa.
Mabaki hayo yatapelekwa kwenye maeneo muhimu kwa maisha ya Lumumba na kuzikwa katika kaburi mjini Kinshasa Juni 30, 2022 baada ya siku tatu za maombolezo ya kitaifa.
