
Raia wa Ethiopia wanapiga kura kuchagua wawakilishi wa bunge la taifa la mabunge ya majimbo.
Uchaguzi huo unaofanyika hii leo, unaelezwa kuwa ni mtihani mkubwa kwa waziri mkuu wa mchi hiyo, Abiy Ahmed, wakati ambapo vita na masuala ya usimamizi vikizuia kura kupigwa katika majimbo zaidi ya 100 kati ya 547 nchini kote.
Uchaguzi huo ulioahirishwa kutoka mwaka jana, ndiyo ajenda kuu ya kampeni ya mageuzi ya waziri mkuu Abiy, ambaye kuingia kwake madarakani mwaka 2018 kuliashiria mwisho wa miongo kadhaa ya utawala wa kiimla na kumpelekea kushinda tuzo ya amani ya Nobel.
Abiy ameutaja uchaguzi huo kuwa ni jaribio la kwanza la taifa hilo kuendesha uchaguzi huru na wa haki.
Misururu ya wapigakura imeshuhudiwa katika baadhi ya maeneo ya mji mkuu, Addis Ababa, huku usalama ukiimarishwa katika taifa hilo la pili kwa wakazi wengi, barani Afrika.
