Leo Jumatatu, Septemba 29, 2025, Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuanza rasmi kampeni zake za uchaguzi mkoani Tanga, ikiwa ni mwezi mmoja kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.
Akiwa anatokea mkoani Pwani, Dkt. Samia anatarajiwa kufanya mikutano mitatu mikubwa katika Wilaya za Pangani, Muheza na Tanga Mjini, akihimiza wananchi kuendelea kuiamini CCM kwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kudumisha amani wakati wa uchaguzi.
Katika hotuba zake mkoani Pwani, Dkt. Samia aliahidi miradi kadhaa ikiwemo ujenzi wa uwanja mkubwa wa michezo Msoga wilayani Chalinze, kuongeza huduma za matibabu katika hospitali ya wilaya ya Chalinze, kuboresha miundombinu ya barabara, kukamilisha miradi ya maji na umeme pamoja na kutoa hakikisho la usalama na utulivu siku ya kupiga kura.
Ahadi hizo zimejikita zaidi katika kuboresha huduma za jamii, kusogeza maendeleo kwa wananchi na kuhakikisha kila mtanzania ananufaika na rasilimali za nchi.
Kwa wilaya ya Pangani, CCM imeahidi kupitia ilani yake ujenzi na ukamilishaji wa zahanati saba katika maeneo mbalimbali, ujenzi wa vituo vitatu vya afya, ukarabati wa hospitali ya wilaya, ujenzi wa madaraja kumi, na kuendeleza ujenzi wa barabara ya Tanga–Pangani yenye urefu wa kilomita 50.
Pia CCM imepanga kufunga taa 200 za barabarani ili kuongeza usalama na mwonekano usiku.
Katika Wilaya ya Muheza, ahadi ni pamoja na ujenzi wa shule kumi mpya, stendi kuu ya mabasi, madarasa 330, maabara 20, miradi ya maji katika vijiji zaidi ya 30, pamoja na ufungaji wa taa za barabarani 200.
Kwa upande wa Jiji la Tanga, ilani ya CCM imeweka mpango wa ujenzi wa Kituo cha Afya Kirare, wodi ya dharura katika hospitali ya wilaya, na zahanati mpya katika maeneo ya Machui, Mwarongo, Mpirani na Mapojoni.
Aidha, miradi mikubwa ya kiuchumi imepangwa ikiwemo ujenzi wa gati maalumu la mita 300 kwa shehena za makasha, gati ya mafuta na mafuta ya kula Raskazone, gati la abiria, soko la kisasa Kasera, hoteli ya nyota tano Sahare, soko la Makorora, bandari kavu Pongwe na machinjio ya kisasa.