Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema ndani ya miaka mitano ijayo, endapo chama chake kitapewa ridhaa ya kuunda serikali, watajenga daraja jipya la Jangwani lenye urefu wa mita 390 pamoja na soko kubwa la kisasa katika eneo hilo kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo.
Dkt. Samia amesema hadi sasa taratibu zote za kuanza ujenzi wa daraja hilo zimekamilika, isipokuwa jambo moja dogo linalosubiriwa.
Amesema daraja hilo, mbali na kupendezesha Jiji la Dar es Salaam, litarahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji na hivyo kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Akizungumza leo, Jumatano Oktoba 22, 2025, katika mkutano wa kampeni za Uchaguzi Mkuu uliofanyika Viwanja vya Kecha, Kinyerezi, Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam, Dkt. Samia pia ameahidi ujenzi wa madaraja mengine mkoani humo, ikiwemo daraja la Mzinga, Wilaya ya Ilala.
Ameeleza kuwa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2025–2030 imeelekeza ujenzi wa barabara za juu (flyovers) katika makutano ya Tabata, Buguruni na Fire ili kupunguza msongamano wa magari jijini Dar es Salaam, ambalo ni kitovu cha biashara nchini.
Katika hatua nyingine, Dkt. Samia amesema serikali yake imefanikiwa kujenga upya soko kubwa la kisasa la Kariakoo mara baada ya jengo la awali kuungua moto, na kwamba kwa sasa biashara zinaendelea vizuri katika soko hilo linalohudumia wafanyabiashara na wanunuzi kutoka ndani na nje ya Tanzania.
