Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni, Kinondoni, imewahukumu vijana wanne kifungo cha miaka saba jela kila mmoja baada ya kupatikana na hatia ya kujaribu kumteka mfanyabiashara Deogratus Tarimo, huku washtakiwa wawili wakiachiliwa huru kutokana na ushahidi kutokuthibitisha ushiriki wao.
Waliyoachiwa huru ni Nelson Msela (24), dereva teksi, na Anita Temba (27), baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yao.
Waliohukumiwa ni Fredrick Nsato (21), askari mkazi wa Kibamba, Isaack Mwaifuani (29), bondia kutoka Kimara, Benki Mwakabela (40), wakala wa mabasi Stendi ya Magufuli, na BatoTweve (32), bondia mkazi wa Kimara Bonyokwa.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu
Ramadhan Rugemalila amesema ushahidi wa upande wa Jamhuri umeweza kuthibitisha bila kuacha shaka kwamba washtakiwa hao wanne walihusika katika jaribio la utekaji, ingawa hawakufanikiwa kumteka mwathirika.
Kabla ya hukumu, upande wa mashtaka uliiomba Mahakama itoe adhabu kali kama fundisho kwa jamii, huku washtakiwa wakiomba kupunguziwa adhabu wakidai walidanganywa na Nsato kwamba walikuwa wakisaidia kumkamata mtuhumiwa.
Tukio hilo lilitokea Novemba 11, 2024 eneo la Kiluvya Madukani , Wilaya ya Kinondoni, ambapo inadaiwa washtakiwa walipanga kumteka Tarimo wakitumia mtego uliopangwa na Anitha Temba, aliyemshawishi mfanyabiashara huyo wakutane kwenye hoteli kwa mazungumzo ya biashara.
Baada ya Tarimo kufika kwenye eneo aliloelekezwa, alisubiri kwenye baa kama alivyoambiwa, ndipo washtakiwa walipofika kwa gari aina ya Toyota Raum lenye namba T 237 EGEna kujaribu kumteka, kabla ya mpango huo kushindikana.
